Genesis 1:3-31

3 aMungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. 4 bMungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. 5 cMungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.

6 dMungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” 7 eKwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. 8 fMungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili.

9Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. 10 gMungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema.

11 hKisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. 12Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema. 13Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu.

14 iMungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka, 15nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. 16 jMungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. 17Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, 18 kitawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 19Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.

20 lMungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” 21 mKwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 22 nMungu akavibariki, akasema, “Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” 23Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.

24 oMungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. 25 pMungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wa kufugwa kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.

26 qNdipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”

27 rKwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,
kwa mfano wa Mungu alimuumba;
mwanaume na mwanamke aliwaumba.
28 sMungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”

29 tKisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. 30 uNao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.

31 vMungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.

Genesis 2:1

1 wKwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo.

Copyright information for SwhNEN